Msanii anaefanya vizuri kwa sasa kwenye muziki wa mduara Shilole,
amesema kuwa ndani ya mwaka huu 2012 unaoelekea kuishia tasnia ya muziki
imemlipa kwa kiasi kikubwa na kumpa mafanikio kwa haraka kuliko filamu
tasnia ambayo ndiyo iliyomtambulisha kwa mashabiki.
Alisema kuwa faida kubwa aliyoipata kwenye muziki ni kwamba alikuwa
hakosi show na kila show anayopiga huwa analipwa kiasi kikubwa cha pesa,
tofauti na filamu ambazo hucheza mara moja na kusubiri ifanye vizuri
sokoni.
“Muziki kwa namna moja ama nyingine umejenga maisha yangu kwa kiasi
kikubwa sana naweza kusema ni tasnia ambayo imenipa mafanikio makubwa
sana namshukuru mungu kwa kunipa kipaji cha kuimba na uwezo kila siku,
pia nawashukuru mashabiki wangu kwa kunikubali na tangu nilipotoa wimbo
wangu wa kwanza,” alisema.
Hata hivyo aliulizwa swali kuwa ndani ya mwaka huu amecheza filamu ngapi
za kwake mwenyewe, ndipo alipojibu kuwa hajatoa filamu yake mwenyewe
hata moja na zote alizocheza zilikuwa za kushirikishwa lakini anaamini
hapo mwakani atakuja na project yake mwenyewe ya kutoa movi kutoka
kwenye kampuni yake.
“Ndani ya mwaka huu kwa kweli sijatoa movie yangu mwenyewe na zote
nilizofanya nilikuwa nashirikishwa lakini najipanga kuja na project
yangu mwenyewe hapo mwakani Mungu akipenda na hiyo ndiyo itakuwa safari
yangu mpya kwani nitakuwa natoa kazi kutoka ndani ya kampuni yangu,”
aliongeza.
"MUZIKI UNALIPA ZAIDI KULIKO FILAMU NA MAIGIZO"......SHILOLE

