Jana tulichapisha habari ya kutia hofu
na iliyoashiria kwamba upo uwezekano mkubwa wa wananchi wengi kupoteza
maisha wakati wowote kutokana na Sekta ya Ujenzi kuendeshwa kiholela na
bila usimamizi wa viwango. Kampuni ya Design Plus Archtects (DPA),
ambayo ilipewa zabuni ya kufanya ukaguzi wa majengo katika Manispaa ya
Ilala, jijini Dar es Salaam imegundua kuwa, kati ya majengo ya ghorofa
90 yaliyokaguliwa katika manispaa hiyo, 67 yamejengwa chini ya kiwango
na kinyume na sheria.
Msemaji wa kampuni hiyo ya DPA, Mustafa
Maulid aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi kwamba
hali ni mbaya katika majengo waliyoyakagua, huku akisema majengo hayo
yana nyufa nyingi na yanaweza kuporomoka wakati wowote. Uamuzi wa kuipa
kampuni binafsi kazi ya kukagua majengo ulikuja baada ya jengo lenye
orofa 16 katika manispaa hiyo kuanguka Machi 26, mwaka huu na kuua watu
36, mbali na majengo mengine yaliyoanguka na kusababisha maafa makubwa
huko nyuma.
Tunasema hizi ni habari za kutia hofu
kutokana na ukweli kwamba hali hiyo mbovu ya majengo siyo tatizo la
Manispaa ya Ilala pekee, bali pia ndiyo hali ya majengo katika maeneo
mengi ya miji yetu hivi sasa. Sekta ya Ujenzi katika nchi yetu katika
miaka ya hivi karibuni inaweza kufananishwa na mtoto yatima aliyeachwa
duniani pasipo usimamizi au matunzo stahiki ya kumfanya aishi maisha ya
heshima na katika mazingira yasiyo ya udhalilishaji. Hofu pia inatokana
na mamlaka zilizopewa dhima ya kusimamia Sekta ya Ujenzi kushindwa
kufanya hivyo kutokana na kugubikwa na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Kariakoo ni eneo kubwa lenye msongamano
mkubwa wa watu, kwani ndio kituo chenye mkusanyiko wa watu kutoka wilaya
zote za Mkoa wa Dar es Salaam na sehemu nyingine, ikiwamo Zanzibar.
Tunaambiwa hata kama siyo mtaalamu wa ujenzi, ukipita Kariakoo utagundua
kwamba majengo mengi ya ghorofa yamejengwa bila kuzingatia sheria za
ujenzi.
Hali hiyo imethibitishwa pia na Kampuni
ya DPA iliyofanya ukaguzi wa majengo katika Manispaa ya Ilala. Kampuni
hiyo inasema imegundua watu wengi wanafanya ujenzi bila vibali,
wanajenga bila kufuata michoro iliyoidhinishwa na Manispaa ya Ilala na
watu wanahamia kwenye majengo ya ghorofa kabla ujenzi wake
haujakamilika. DPA pia inasema majengo yanatofautiana na michoro
iliyotoka kwa wataalamu husika. Kwa mfano, pamoja na majengo yote ya
Kariakoo kutakiwa kuwa na maegesho ya magari, wajenzi wameweka fremu za
maduka.
Bahati mbaya hata Meya wa Manispaa ya
Ilala, Jerry Silaa hana jibu sahihi kuhusu nini kifanyike. Kwa kudhani
kwamba vikao vya madiwani ndivyo vitakavyotoa jibu kuhusu tatizo hilo,
Meya Silaa anaonyesha bayana kwamba hata yeye hajui ukubwa wa tatizo
hilo. Pamoja na kwamba kisheria madiwani ndio wenye dhima ya kusimamia
sera za ukuaji wa miji, matatizo yaliyobainishwa na DPA ni mazito mno
kutatuliwa na madiwani hao.
Sisi tunadhani mamlaka ya kufanya uamuzi
mgumu kuhusu ghorofa nyingi mbovu za Kariakoo na kwingineko ni Serikali
Kuu, ambayo pamoja na mambo mengine inapaswa kuwawajibisha walioshindwa
kuzuia ujenzi holela. Hapa tuna maana kwamba uamuzi huo ufanywe na
Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Rais mwenyewe.
NANI AWAJIBIKE UJENZI WA MAGHOROFA MABOVU KARIAKOO....!

