INATISHA sana! Renard Mabula, mkazi wa Kiluvya jijini Dar es Salaam
amekufa ndani ya Kituo cha Polisi cha Gogoni, Kinondoni jijini Dar es
Salaam baada ya kukimbilia hapo kufuatia kuchomwa kisu tumboni na mtu
aliyetajwa kwa jina la Moleli (22), Uwazi lina mkanda kamili.
Kwa mujibu wa habari za kipolisi, tukio hilo lilijiri Februari 11,
mwaka huu, Gogoni ambako ndiko kwenye makazi ya mtuhumiwa na marehemu
huyo.
Awali ilidaiwa kuwa, marehemu huyo alikuwa akidaiwa shilingi elfu
tano na Moleli lakini alikuwa akimzungusha kwa muda mrefu bila kumlipa.
“Siku ya tukio, Moleli alikwenda kwa marehemu kumdai fedha zake hizo
na kujibiwa kuwa, kwa muda ule hakuwa na kitu ndipo, Moleli akaamua
kumchoma kwa kisu tumboni.
“Marehemu kuona vile huku akivuja damu kwa wingi alikimbilia Kituo
Kidogo cha Polisi cha Gogoni Kiluvya. Alipofika alisimulia mkasa wake
lakini alipomaliza tu akakata roho, mwili wake ukapelekwa Hospitali ya
Tumbi, Kibaha, Pwani ambapo madaktari walithibitisha kuwa alishafariki
dunia,” kilisema chanzo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baba mzazi wa mtuhumiwa huyo (jina
tunalo) alisema analishangaa sana Jeshi la Polisi Kituo cha Mbezi ambapo
mtoto wake alipelekwa kutoka kituo kidogo cha Gogoni baada ya
kutuhumiwa kwa mauaji ya Mabula lakini aliachiwa huru.
Akaendelea: ‘’Mimi mwenyewe huyo mtoto wangu alishawahi kunitishia
kuwa atanichoma kisu baada ya kumtaka aende shule. Tumemshauri mara
nyingi na mama yake lakini hataki kusikia, sijui ni mtoto gani
asiyesikia wazazi?’’ alihoji baba huyo.
Wakati hayo yakitokea, mwanamke mmoja wa eneo hilo aliyejitambulisha
kwa jina la Getruda Athanas (36), yuko shakani akidai kwamba, Molel
amekuwa akimtishia kumchinja kwa kisu baada ya kumtuhumu kuiba kuku
wake.
Mwanamke huyo alikimbilia Kituo cha Polisi Gogoni na kufungua malalamiko kwa kumbukumbu KLV/RB/521014 KUTISHIA KUUA KWA MANENO.
Akizungumza na Uwazi, Getruda alisema: “Nilipomuuliza kama kweli aliiba
kuku wangu, alikiri akidai alitaka apate fedha. Lakini akaniambia
nikiendelea kumfuatilia atanichinja, akitoa mfano wa jinsi alivyomuua
Mabula kwa kisu.”
Uwazi lilimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camilius Wambura na kumuuliza kuhusu taarifa hizo ambapo alikiri.
Uwazi: Sasa afande ililkuwaje mtuhumiwa akakamatwa na kuachia huru?
Kamanda: Nimeshamwagiza kamanda wa polisi wa wilaya ‘OCD’ (hakumtaja jina) kufuatilia madai ya mtuhumiwa kuachiwa huru.
ACHOMWA KISU NA KUFIA POLISI KISA DENI LA TSH 5000/=

