Msanii wa kike anayefanya poa kwenye game kutoka pande za Zenji Baby J, amefanya mahojiano maalumu na mwandishi wa makala hii
na kusema kuwa ndani ya mwaka huu amejipanga kikamilifu ikiwa pamoja
na ujio wa mzingo wake mpya anaomalizia kufanya na msanii Diamond unaokwenda kwa jina la ‘Nimempenda Mwenyewe’.
Baby J alisema
kuwa ujio wa ngoma hiyo utakuwa wa kipekee kwani amejipanga kwa lengo la
kufanya kazi kwa sababu tayari amekua kiakili, mawazo na hata kimuziki
baada ya kufanya kazi kibao ndani ya mwaka uliopita ambazo zimempa
nafasi kubwa ya kujiamini zaidi.
Alisema kuwa sambamba na ujio wa ngoma hiyo pia suala la wasanii wengi
kutoka Zanzibar na kuja kufanya muziki Tanzania Bara linatokana na aina
ya muziki ambao umekuwa ukifanywa visiwani humo ambao ni taarabu na
hivyo miziki ya kisasa inaonekana ya kihuni kutokana na maandali
yaliyomo visiwani humo.
Alisema kuwa sambamba na maandili pia Zanzibar ni ndogo
hivyo wanalazimika kuja DSM, ingawa kwa upande mwingine wamekuwa
wakipokelewa vizuri na mashabiki wa Zanzibar kutokana uwakilishi wao.
“Naweza kusema Zanzibar muziki ambao umekuwa ukijulikana zaidi ni
taarabu na mingine ya asili hivyo aina ya mizki yetu sisi haipewi nafasi
sana kutokana na maadili kwani muziki wetu unaonekana unavunja baadhi
ya maadili lakini hata hivyo si kwamba hauna soko bado unapokelewa
vizuri,” alisema.
Baby J
alizungumzia suala la kutotoa albamu ambapo alisema kuwa kwa upande
wake hawezi kuachia albamu ingawa ana ngoma nyingi ambazo zinaweza
kufika hata albamu mbili, lakini anaona ni vizuri kutoa single kwani
ndizo zinazolipa vizuri kwa sasa.
Juu ya kufanya kazi za nje alisema kuwa ana mipango ya kufanya ngoma na msanii wa Kenya Amani,
alidai ni nyota ambaye amekuwa akimkubali toka kitambo, hivyo ndani ya
mwaka huu atakuwa amefanya naye kazi ingawa wapo pia wasanii wengine wa
nje ya Tanzania anaotarajia kushirikiana nao.
BABY J AZUNGUMZIA KUHUSU UJIO WA NGOMA YAKE MPYA PAMOJA NA USIRI WA NDOA YAKE

