Mwaka Mpya wa 2013 umeanza taratibu,na matukio mengi yametokea mwaka 2012.
Anga la burudani hususan muziki wa Bongo Fleva liligubikwa na matukio kadha wa kadha, wapo wakongwe waliondeleza ukongwe wao lakini wapo ambao wamefanya vizuri na kuufanya mwaka 2012 kuwa na mafanikio katika upande wa shoo, kujulikana na kipato ambapo tunaweza kusema ulikuwa mwaka wao.
DIAMOND:
Nyota yake ilivuka mipaka mwaka 2012, akang’aa zaidi na amepata mafanikio makubwa kwa kupiga shoo nyingi pengine kuliko wasanii wote ndani ya Bongo Fleva. Jina lake limekuwa gumzo maradufu.
OMMY DIMPOZ:
Mwaka 2012 jamaa alipata mafanikio makubwa ya ghafla, ndani ya muda mfupi ameweza kutambulika na Watanzania. Levo ya muziki wake imeweza kufananishwa na muziki ambao unafanywa wasanii wakali wa Nigeria kama akina P-Square. Amefanya shooting ya wimbo wa Baadaye pande za Afrika Kusini kwa gharama kubwa, amefanya shoo nyingi kwa kipindi kifupi.
RICH MAVOCO:
Shavu kubwa alilipata kupitia shoo za Serengeti Fiesta 2012. Amekubalika sana kupitia wimbo wake wa Marry Me, amepata shoo nyingi zaidi na jina lake kuwa juu. Alitajwa kuwa miongoni mwa wasanii ambao pengine wangeweza kumpoteza Diamond ambaye kidogo alionekana kupoa.
LINNAH:
Chimbuko lake ni Jumba la Vipaji Tanzania (THT). Amefanya vizuri sana kulijenga jina lake kwa mwaka 2012 kiasi cha mashabiki kuanza kuhisi ndiye mrithi wa wakongwe kama Lady Jaydee na Ray C. Amepata shoo mbalimbali, ndani na nje ya nchi na jina lake limekua gumzo kwa wadada wanaoimba Bongo Fleva.
STAMINA:
Hili ni jembe lililokomaa kwenye muziki wa Hip Hop Bongo. Shoo zake kwenye matamasha ya Fiesta 2012, zimeleta mapinduzi makubwa. Amepata mafanikio makubwa ya kujenga jina lake, limekubalika na kila mtu akaanza kutambua mrithi wa Fid Q amepatikana, akapata dili nyingi za shoo.
SHETTA:
Kwa sasa anapenda umuite Bonge la Bwana, mafanikio yake yamechomoza harakaharaka, kila mtu akakubali staili yake ya kucheza na maneno. Mwaka 2012, amejizolea umaarufu mkubwa kwa mashabiki, akapata shoo nyingi mjini. Kistaili chake cha Okeee! kimekuwa gumzo kwa mashabiki

RECHO:
Ni zao la Jumba la Vipaji Tanzania (THT) ambaye mwaka jana nyimbo zake zikipendwa na kupigwa mara nyingi katika vituo mbalimbali vya redio. Amefanya shoo nzuri katika jukwaa la Fiesta 2012, Watanzania walimuunga mkono kwa kutoa shangwe kubwa kila alipokuwa jukwaani.
IZZO BUSINESS:
Alileta upinzani mkubwa kwenye gemu la muziki wa Hip Hop. Nyimbo zake zilikuwa na mguso kwa jamii. Wimbo wake wa Riz-One ulimpa umaarufu mkubwa na kumfanya apate shoo nyingi ikiwemo ile iliyofanyika katika Ukumbi wa Dar Live akiwa na R.O.M.A. aliyetikisha ndani na nje ya Bongo hadi akatwaa Tuzo za Msanii Bora wa Hip Hop na Wimbo Bora wa Mwaka 2012.
GODZILLAH:
Alianza kwa staili kama rapa wa Marekani, 50 Cent. Ilichukua muda hadi Watanzania kumuelewa. Baada ya kutoa nyimbo kadhaa, mafanikio yalianza kuonekana kupitia shoo zake. Umati ulilipuka kwa shangwe, pato lake likaongezeka kiasi cha kumwezesha ajiunge katika Chuo cha Biashara cha CBE, jijini Dar. Jina lake limevuka mipaka ya mikoa yote ya Tanzania.