Katika
harakati za kusaka wenzi, vijana wengi wamekuwa wakibabaika juu ya sifa
za mwenzi ambaye anaweza kuwa sahihi katika maisha yake. Hili limekuwa
tatizo sugu hasa kwa vijana wengi!
Lakini vijana wa sasa huhadaika
zaidi na mvuto wa sura na maumbile ya mtu wakifanya kama kipimo kikuu
cha anayefaa kuwa mwenzi wa maisha, jambo ambalo ni makosa makubwa sana.
Kudanganyika
na uzuri wa nje pekee siyo kati ya sifa muhimu zaidi za kumfanya awe na
sifa za kuwa mwenzi wako wa maisha. Zamani, wazee wetu walikuwa
wanatizama kwanza heshima na uchapakazi kama vipimo vya awali vya kumpa
sifa mwanamke kuolewa. Siku hizi ni kinyume chake.
Lakini inashauriwa
kuwa makini sana na uchaguzi wako wa mke/mume kwani kufanya maamuzi
yasiyo sahihi ni sawa na kujirudisha mwenyewe nyuma. Kuwa na msimamo,
fanya uchaguzi ulio sahihi, ambao hautakufanya baadaye ujutie!
Kitu
cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kuhakikisha unakifikiria ni juu ya
mapenzi yako kwake! Sema na moyo wako ukupe ukweli juu ya hilo,
usikurupukie mapenzi, usije ukamuona msichana siku moja amevaa suruali
inambana kiasi cha kuonyesha umbile lake halafu ukamtamani ukadhani
unampenda, utakuwa unapotoka!
Mapenzi siyo kitu cha mchezo, huanza
moyoni jiridhishe kwanza ndipo ukubali kumwingiza katika moyo wako.
Kumbuka kuwa unapoamua kufunga ndoa na mtu ni ahadi ambayo mmeahidiana
mbinguni na duniani, ni ahadi ambayo inapaswa kutenganishwa na kifo tu,
siyo vinginevyo! Kamwe usifanye majaribio katika mapenzi, mapenzi
hayajaribiwi!
Kitu cha pili ambacho unatakiwa kukiangalia ni kuhusu
mapenzi yake ya kweli kwako. Wataalam wa Mambo ya Mapenzi wanasema,
ingawa ni vizuri kuishi na mtu unayempenda lakini pia ni lazima awe
anakupenda! Siyo vigumu sana kumfahamu mwenzi anayekupenda, lakini pia
inawezekana ukaona anakupenda kumbe ni danganya toto!
Kimsingi katika
hili ni lazima utumie akili yako yote uweze kutambua hilo. Katika
makala zangu zilizopita nilianisha sifa za mpenzi mwenye mapenzi ya
dhati, lakini kwa kuongezea ni kwamba, anayekupenda huwa mvumilivu,
anayekusikiliza pia mwenye kuwajali ndugu, marafiki na jamaa zako,
anayekuheshimu na kutambua thamani yako!
Anayetakiwa kuwa mwenzi wako
wa maisha lazima awe makini na mwenye akili za kimaisha. Siyo lazima
awe na elimu ya darasani, haijalishi ni mwanamke aliyekulia vijijini au
mjini, lakini hapa tunaangalia uwezo wake wa kufikiri. Hata
hivyo, inategemea wewe umepanga kuishi na mwanamke wa
aina gani, lakini mwanamke ninayemzungumzia hapa ni yule mwenye uwezo wa
kutosha wa kufikiri na kupambanua mambo. Wiki ijayo tutaendelea,
USIKOSE!
JE......VIGEZO VYA UTANASHATI, FIGA LA ADABU NDO KILA KITU?

