KATIKA hali iliyoonesha
sintofahamu, jina la utani la Mbunge wa Mbeya Mjini kwa ‘leseni’ ya
Chadema, Mhe. Joseph Osmund Mbilinyi ‘Sugu’ lilionekana kumtatiza Spika
wa Bunge la Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda.
Ilikuwa wakati
Mbilinyi akizungumza kwa niaba ya kambi rasmi ya upinzani kuchangia
bajeti ya Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo ya Mhe. Fenella
Mukangara ndipo alipotibua mambo yaliyosababisha spika atatizwe na jina
lake la Mbilinyi.
Mhe. Mbilinyi alipofika ukurasa wa nane wa hotuba
yake yenye kurasa 54, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Mhe. Godfrey Zambi
(CCM) aliomba mwongozo (kuomba mwongozo ni kumtaka anayehutubia kuacha
na kurudi kwenye kiti kisha aliyeomba aongee).
Ndipo Spika Makinda alipomtaka Mhe. Mbilinyi akatishe hotuba yake ili Zambi azungumze.
Hata hivyo, Mbilinyi aliendelea kutiririka kwa sekunde kadhaa kabla ya kutii amri ya spika.
Ilimlazimu
spika kumwambia tena akisema: “We mheshimiwa Sugu…” kauli iliyoamsha
kicheko kwa wabunge huku Sugu mwenyewe akiwa ameondoka kwenye kipaza
sauti huku akimwekea spika alama ya vidole viwili inayotumiwa na
Chadema.
Mhe. Zambi alitoa hoja kuhusu hotuba ya Sugu kujaa maneno ya uchochezi.
Spika
Makinda kwa uwezo wake aliamua kuliahirisha bunge mpaka saa 10:00 jioni
ya siku hiyo akimtaka Sugu kwenda kuondoa maneno yenye uchochezi katika
hotuba yake.
Jioni ilipofika, Sugu akapewa nafasi ya kuzungumza
ambapo alianza kwa kusema: “Mheshimiwa spika, natamka ndani ya bunge
kwamba kuanzia leo jina la Sugu lisitumike.”
Spika akadakia hapo na kusema: “Tena imekuwa afadhali maana mi mwenyewe sijui ni Sugu au Suguru.”
Kauli hiyo ya Spika Makinda ilisababisha wabunge waangue vicheko.
JINA LA SUGU LAPIGWA MARUFUKU KUTUMIKA BUNGENI..

