Rais Jakaya Mrisho Kikwete
(yumo garini kushoto) akikagua sehemu ya kutua na kupaa ndege ya uwanja
wa Tabora jana Januari 10, 2013 mara baada ya kuzindua rasmi ujenzi wake.
Rais Jakaya
Mrisho Kikwete akiongea na balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe
Radhia Msuya mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Kimataikfa wa
Julius Nyerere jijini Dar
es salaam akitokea mkoani Tabora alikokuwa katika ziara ya kikazi ya
siku tano kukagua shughuli za maendeleo na kuzindua miradi mbalimbali.
Waziri wa Ujenzi Dkt John
Pombe Magufuli (kulia) na Waziri wa Uchukuzi Dkt Harrison Mwakyembe
wakiongea wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Tabora jana Januari 10, 2013 .
(PICHA NA IKULU)
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI YALIFUFUA SHIRIKA LA RELI TANZANIA
SERIKALI imetangaza hatua kubwa na kabambe za kufufua usafiri wa
abiria na mizigo, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabehewa na injini za
treni, katika hatua kubwa za aina yake kuchukuliwa na Serikali kwa muda
mrefu katika kurekebisha usafiri wa treni nchini.Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Harrison George Mwakyembe ametangaza hatua hizo leo, Alhamisi, Januari 10, 2013, wakati alipokuwa anamkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka jiwe la msingi kwenye ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Tabora ikiwa ni tukio la mwisho la ziara yenye mafanikio makubwa ya siku tano ya Rais Kikwete katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete na mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe ya uwekaji jiwe hilo la msingi kwenye Uwanja huo kuwa Wizara yake imeanza kubadilisha reli nyepesi, iliyochakaa na yenye uzito mdogo kwa Reli ya Kati.
Amesema kuwa kwa kupitia mashirika yake ya RAHCO na Shirika la Reli Tanzania (TRL) Serikali itafanya marekebisho hayo makubwa njia mzima ya Reli ya kati na kuwa mafundi wa mashirika hayo tayari wamefika Mkoa wa Morogoro.
Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa Serikali kupitia Wizara yake na mashirika yake hayo, imeagiza mabehewa mapya ya mizigo 274, imeagiza mabehewa mapya ya abiria 22, imeagiza mabehewa mapya ya kubebea kokoto 25 na pia imeagiza mabehewa ya breki (brake vans) 34 na tayari malipo ya awali yamefanyika.
Katika namna inayothibitisha dhamira ya Serikali kurekebisha hali ya usafiri wa reli nchini, Mheshimiwa Mwakyembe pia amewaambia wananchi kuwa Wizara yake pia imeagiza crane mpya na kubwa ya kubebea mizigo yenye uzito unaofikia kilo 100.
Kuhusu injini za treni, Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete kuwa zabuni kwa ajili ya kutengeneza upya (re-manufacturing) injini nane za treni imetolewa ili utengenezaji huo ufanyike, iwe ni ndani ama nje ya nchi.
Pia Waziri amesema kuwa oda imetolewa kwa ajili ya utengenezaji wa injini mpya 13 za treni ambazo malipo yake yatafanyika katika mwaka ujao wa fedha hata kama utengenezaji wa injini hizo utaanza.
Aidha, Waziri amesema kuwa Wizara kupitia mashirika yake hayo mawili imeagiza spea za kutosha kuweza kufanya ukarabati mkubwa wa injini tano kwenye karakana zilizoko hapa nchini.
“Mheshimiwa Rais, kwa hesabu nyepesi tu ni kwamba katika kipindi kifupi tutaweza kuwa na injini kiasi cha 26 ambazo zitarudisha uhai wa usafiri wetu wa reli kwa kiasi kikubwa sana,” Waziri Mwakyembe amemwambia Rais Kikwete.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
10 Januari, 2013