NAMSHUKURU
Mungu kwa kunikutanisha nanyi tena kupitia ukurasa huu namba moja kwa
kuandika makala nzito zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Wiki
iliyopita utakumbuka nilianza kuzungumzia tabia ya baadhi ya watu
kuwakaripia wapenzi wao mbele za watu bila kujua kuwa kufanya hivyo
madhara yake ni makubwa sana.
Ninachokizungumzia ni wapenzi kuheshimiana na kutovunjiana heshima kwa kusemana vibaya mbele za watu.
Katika
hilo naomba nisisitize kwamba, kukaripiana ovyo kunapunguza mapenzi pia
kunatoa mwanya kwa vidudu watu kupenyeza maneno yatakayomkera mmoja
wenu na mkajikuta kila siku ni watu wa kuwapa watu sinema ya bure.
Tunapokuwa
kwenye uhusiano tunatakiwa kujenga picha nzuri kwa wanaotuzunguka.
Tusiwafanye watuone sisi kama wahuni tunaopelekana kama watu waliovuta
bangi.
Itakuwa si jambo jema kama mpenzi wako au mkeo kakuudhi
ukaanza kumsema mbele ya mashoga zako tena wakati mwingine na matusi
juu. Ukifanya hivyo kwanza utaonekana mshamba lakini pia utawafanya watu
wahisi kuwa uhusiano wenu upo upo tu.
Wanaopendana kwa dhati
wanachagua wapi pa kusema nini kwa mpenzi, wanajua umuhimu wa kufichiana
upungufu wao. Hivi leo hii mkeo akukute upo na marafiki zako kisha
aanze kukusema jinsi ambavyo jana yake hukumfurahisha faragha, inaingia
akilini kweli?
Hapo mwanamke atakuwa anatatua tatizo au analiongeza?
Kwa kifupi atakuwa analiongeza kwani atakuwa amezidi kumuathiri mumewe
kisaikolojia.
Ndiyo maana nasema, wapenzi walio kwenye uhusiano
thabiti, hawasemani ovyo. Hawa wanajua sehemu maalumu ya kuwekana sawa
na hata lugha inayofaa kutumika kurekebishana kwani lengo ni kujenga na
si kubomoa.
Kwa maana hiyo tujiepushe sana na tabia mbaya ya
kukoromeana mbele za watu tukiamini kwamba kufanya hivyo ni kuboresha
uhusiano wetu lakini pia tunajenga misingi ya kuheshimiana na kupendana
kwa dhati.
Pale ambapo inatokea mmoja kamkosea mwenzake ni vyema
akaomba msamaha kwa unyenyekevu na kuonyesha kujutia kosa lake kisha
kuyaacha maisha yenu ya furaha na amani yaendelee kuwepo. Usione ugumu
kumwambia mpenzi wako; ‘samahani mpenzi wangu….’
Ukifanya hivyo hata
yeye atakapokukosea atakuomba msamaha na hiyo itawafanya mzidi kupendana
na kuheshimiana. Tatizo ni kwamba kuna baadhi ya watu wanapowakosea
wapenzi wao hawataki kuonekana ni wakosaji.
Ukiwa hivyo usishangae
ukawa mtu wa kubalaswa na mpenzi wako kila mara na kweli anaweza kufikia
hatua ta kukuvunjia heshima mbele za watu akidhani ndiyo dawa yako.
Naomba
nihitimishe mada hii kwa kusema kwamba, unapoingia kwenye uhusiano
jitahidi sana kutomkera mpenzi wako mara kwa mara. Ni kweli kuna wakati
unaweza kufanya jambo bila kudhamiria na likamtibua lakini isiwe kila
mara.
Hakikisha unakuwa mstari wa mbele katika kuliboresha penzi
lenu. Kuwa mtu wa kumfanyia mpenzi wako mambo ya kumfurahisha, pale
unapobaini umemkera jirudi haraka ili usiharibu hali ya hewa.
Kwa leo ni hayo tu, tuonane wiki ijayo.
GP.
HATA KAMA KAKUKOSEA, KUMKARIPIA MBELE ZA WATU NI KUMDHALILISHA!-2

