KARIBU
sana katika makala yetu inayohusu afya.Kutokana na simu nyingi
ninazozipata nikiulizwa maswali juu ya maumivu yanayowapata akina mama
wengi wakati wa hedhi nimeona ni bora niandike makala hii ili iweze
kuwasaidia na wengine kujua nini chanzo na mhusika afanye nini pale
anapopatwa na tatizo hilo.
Maumivu wakati wa hedhi (period
pains) au kitaalamu dismenorrhea, ni maumivu yanayojitokeza sehemu ya
chini ya tumbo au kiunoni wakati mwanamke anapoanza kupata siku zake au
kabla ya hapo.
Maumivu hayo huweza kuwa madogo au ya wastani huku
baadhi ya wanawake wakipata maumivu makali sana. Maumivu hayo huanza
pale yai linapotoka katika mrija (fallopian tube) na kuteremka chini ya
mrija huo wakati wa Ovulation.
AINA YA MAUMIVU
Maumivu ya tumbo la hedhi yapo ya aina mbili. Ya
kwanza ni maumivu yasiyokuwa na sababu zozote za kimsingi za kitiba.
Katika aina hii maumivu ni ya kawaida na huhisiwa sehemu ya chini ya
tumbo na kiunoni. Maumivu hayo huanza siku moja au mbili kabla ya hedhi
na humalizika baada ya siku mbili au nne.
Aina ya pili ni yale
maumivu yanayojumuisha maumivu yanayosababishwa na sababu nyinginezo za
kitiba kama vile matatizo katika kizazi, ugonjwa wa nyonga (PID) na
matatizo katika mirija ya mayai.
Nusu ya wasichana na wanawake hupata
maumivu wakati wa hedhi na karibu asilimia kumi mpaka kumi na tano
wanasema kuwa hupata maumivu makali.
Uchunguzi unaonesha kuwa kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuongeza uwezekano wa kuumwa tumbo wakati wa hedhi.
Sababu
hizo ni kama kuwa na umri wa chini ya miaka 20, kuvunja ungo wakati wa
miaka 11 au chini ya miaka hiyo, kutoka damu nyingi wakati wa hedhi,
wanawake ambao hawajawahi kuzaa.
Magonjwa yanayoweza kusababisha mtu kupatwa na maumivu ya tumbo la hedhi. Miongoni mwa magonjwa hayo ni:
Endometriosis. Hii ni hali ambayo seli za ndani ya mfuko wa uzazi huanza kuoka nje ya fuko hilo, au hata sehemu nyinginezo
Adenomyosis: Huu ni ugonjwa wa wanawake ambapo tezi au uvimbe (tumors) zinaota katika mfuko wa uzazi.
PID au Ugonjwa wa uvimbe katika nyonga.
Magonjwa ya zinaa yanayotokana na bakteria au magonjwa ya kuambukiza ya zinaa.
Mlango wa uzazi unapokuwa mdogo kiasi kwamba unazuia damu ya hedhi isitoke kwa urahisi.
Itaendelea wiki ijayo.
KUUMWA TUMBO WAKATI WA HEDHI

