Hakuna
njia mbadala wa kuyachekea mapenzi zaidi ya kuwekeza upendo pale ambapo
unahitaji kupendwa. Ni kichekesho kwa mbaguzi, mwenye chuki kwa wenzake
halafu eti anataka apendwe.
Kosa kubwa ambalo wengi wetu hulifanya
ni kujenga matarajio. Kila mmoja wetu anataka afanyiwe mengi lakini yeye
mwenyewe huwa hajiulizi ni kipi anachopaswa kufanya kwa lengo la
kumridhisha mwenzake. Ni vizuri kujua kuwa kadiri wewe unavyotaraji
kufanyiwa na mwenzako anatarajia umfanyie.
Katika mapenzi hutakiwi
kuingia na sura bandia. Kila ‘aliyefeki’ uhusika wake kwenye uhusiano wa
kimapenzi, aliishia kuharibikiwa. Hata kama una udhaifu wako, acha
uonekane ili uwe huru muda wote. Vinginevyo, utajichimbia kwenye dunia
ya mateso ya kujitakia.
Kukubali udhaifu wako uonekane, kunakupa sifa
kwamba wewe ni mwelewa. Hilo ni jambo la muhimu kuliko kujionesha wewe
ni mkamilifu, halafu baadaye yale uliyokuwa unayaficha yanaonekana, sasa
inakuwa aibu kwako. Mtu bandia kila siku hufeli, mwenye uhalisi wake
atazidi kwenda mbele.
Uhusiano wa kimapenzi siyo kitu rahisi. Huweka
wazi kila kitu ambacho mtu anakifikiria ndani yake au anachokitarajia.
Kwa kawaida, mtu anavyohusika kwenye mapenzi ndivyo ambavyo hutoa
kielelezo cha namna anavyotaka maisha yake na mwenzi wake yawe.
Mapenzi
yanakutaka uwe unatabasamu ili na yenyewe yatabasamu kwa ajili yako.
Huwezi kuwa kwenye kipindi kibaya halafu ukayatendea haki mapenzi. Ukiwa
na siku mbaya, watu wanaokuzunguka, hususan mwenzi wako atakugundua.
Vivyo hivyo, ukiwa hauna furaha.
Ukiwa mtu wa kulia, yenyewe yatalia
na wewe na hutayafurahi hata siku moja. Watu jasiri ambao huamini katika
mapenzi yanayochanua, badala ya kulia, huangalia tatizo na kulipatia
ufumbuzi ili waweze kucheka kisha mapenzi nayo yawachekee.
Tukirejea
pale tulipoishia wiki iliyopita kwenye kipengele cha kuchagua mapambano
ni kwamba wapo wale ambao, hata pongezi kwao inaweza kuibua malumbano.
Sasa kwa vile wewe unataka furaha, inakubidi uangalie namna bora ya
kukabili mambo.
Mfano, unamwambia mwenzi wako umependeza, badala ya
kukujibu asante, anaweza kukuuliza: “Kwani siku nyingine huwa
sipendezi.” Ukimjibu huwa anapendeza, atakuhoji ni kwa nini huwa
humsifii, badala yake umemsifia siku hiyo.
Pengine badala ya kupokea
pongezi, yeye akajibu: “Ni kawaida yangu.” Vilevile, inawezekana
akakuhoji maswali mpaka ukakoma siku nyingine kumpongeza kwa kupendeza.
Hayo ni mambo ambayo unapaswa kuamua ama kuyarekebisha au kuyakimbia
kama utakuwa unataka furaha katika uhusiano wako wa kimapenzi.
Huo ni
mfano tu lakini angalizo kwako ni kwamba uamuzi wa kukimbia ni sawa
lakini huyo ambaye utakutana naye ni binadamu, naye utamkuta ana kasoro
zake, kwa hiyo utatakiwa uamue kuainisha upungufu alionao kabla ya
kuchagua mapambano na mbinu za kupambana. Usikimbie, hebu tulia na
ufanye juu chini kumbadilisha.
Hata hivyo, wakati ukimbadilisha
jaribu kujiuliza maswali ambayo yana msaada mkubwa sana kwako
unapoyapatia majibu. Ainisha vitu vinavyokukwaza kwa mwenzi wako halafu
jiulize kabla hujaingia rasmi kwenye mapambano ya kuyaondoa hayo mambo
yanayokukwaza ili uyafurahie mapenzi yako.
Kuna maswali matatu ya
kujiuliza. Haya kama dira yako lakini kama unadhani yapo mambo mengine
ambayo yanajitokeza kwenye uhusiano wako na unapaswa kujiuliza na kupata
majibu kwa haraka. Sababu ya kujiongeza maswali ni kwamba kuna
mazingira hutofautiana kati ya uhusiano mmoja hadi mwingine.
Itaendelea wiki ijayo.
gpl
UTAMU AU MATESO YA MAPENZI HUTOKANA NA MTINDO WAKO WA MAISHA - 6

